ADDIS ABABA : Uchaguzi wa Ethiopia wazusha wasi wasi
16 Aprili 2005Umoja wa Ulaya leo hii umeelezea wasi wasi wake juu ya repoti za unyanyasaji nchini Ethiopia kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi ujao katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Rob Vermas balozi wa Uholanzi anayeiwaklisha Umoja wa Ulaya nchini Ethiopia amesema wakati akiwakaribisha waangalizi wa uchaguzi 50 wa Umoja wa Ulaya waliaowasili nchini humo hapo jana kwamba repoti za unyanyasaji,watu kutupwa gerezani na vitendo vyengine vya vitisho ni mambo ya kutiliwa wasi wasi.
Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema uamuzi wa serikali ya Ethiopia hapo tarehe 30 Machi kuyatimuwa makundi matatu ya kutetea demokrasia ya Marekani ni wa kukatisha tamaa.
Waangalizi 100 wengine zaidi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuwasili nchini humo hapo Mei 10.
Uchaguzi huo ni wa tatu tokea chama tawala cha EPRDF cha Waziri Mkuu Meles Zenawi kuingia madarakani hapo mwaka 1991 ingawa ni mara ya kwanza kuwa chini ya uangalizi wa kimataifa huku kukiwa na malalamiko kwamba waangalizi wa uchaguzi wa ndani ya nchi wamekuwa wakinyimwa kusiko haki nafasi ya kuangalia uchaguzi huo.