Addis Ababa. Uchaguzi kurudiwa nchini Ethiopia katika vituo sita.
21 Mei 2005Tume ya uchaguzi nchini Ethiopia inachunguza madai mbali mbali ya udanganyifu katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili wiki iliyopita. Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa nchini Ethiopia uchaguzi utafanyika tena kesho Jumapili katika vituo sita vya kupigia kura ambako makasha ya kura yamewekwa kura nyingine ama kura hazikuhifadhiwa vizuri.
Tume ya uchaguzi nchini Ethiopia pia imesema muungano wa vyama vya upinzani pamoja na chama tawala vimetoa malalamiko yao dhidi ya udanganyifu huo. Matokeo ya kwanza rasmi yanaonesha ushindi mkubwa kwa upande wa upinzani katika mji mkuu Addis Ababa. Pande zote mbili zimedai kupata ushindi. Serikali ya waziri mkuu Meles Zenawi imepiga marufuku maandamano kwa muda wa mwezi mmoja baada ya kupigwa kura.