Addis Ababa. Rais wa Ivory Coast kubaki madarakani miezi 12 zaidi.
7 Oktoba 2005Viongozi wa mataifa ya Kiafrika wamesema jana kuwa rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo anapaswa kubaki madarakani kwa muda mwingine wa miezi 12 baada ya muda wake kumalizika mwezi huu, ikiwa ni pigo kwa waasi ambao wanataka rais huyo kuondoka madarakani ili kuepusha mkwamo katika hatua za kuleta amani nchini humo.
Taarifa hiyo ya viongozi wa umoja wa Afrika , ambao wanaonekana kuwa ni nguvu kuu ya kuleta amani katika bara hilo, inaweza kuleta hali ya wasi wasi wa kisiasa katika nchi hiyo ya Ivory Coast ambayo imegawanyika kisiasa.
Hali ya wasi wasi wa kuanza tena mapambano katika nchi hiyo ya Afrika magharibi imeendelea kupanda wakati imeonekana wazi kuwa uchaguzi uliopangwa hapo kabla kufanyika Oktoba 30 kuwa hautaweza kufanyika.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano uliofanyika kwa muda wa saa nne wa baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika uliohudhuriwa na rais wa Afrika kusini Bwana Thabo Mbeki na rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo imeeleza kuwa Gbagbo anapaswa kuhamisha baadhi ya madaraka yake kwa waziri mkuu mpya , ambaye taarifa hiyo imesema atakuwa na mamlaka kamili juu ya mawaziri .
Baraza hilo la amani na usalama la umoja wa Afrika limeeleza haja kubwa ya kuunganishwa tena kwa Ivory Coast haraka iwezekanavyo.