ADDIS ABABA. Mvutano washtadi kati ya Ethiopia na Eritrea.
4 Novemba 2005Milio ya bunduki imesikika tena leo mjini Addis Ababa katika siku ya nne ya mapambano baina ya polisi na wafuasi wa upinzani.
Habari zinasema polisi walipiga risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwapo karibu na makao makuu ya Umoja wa Afrika.Waandamanaji hao wanapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mnamo mwezi mei.Habari zaidi zinasema kwamba vijana kadhaa wamekamatwa.
Vifo vya watu zaidi ya 40 vimethibitishwa na duru za hospitali .
Marekani imetoa mwito wa kurejea katika utulivu na imeitaka serikali ya Ethiopia iondoshe vizingiti dhidi ya vyama vya upinzani na iunde tume huru ili kuchunguza sababu za matukio hayo ya umwagaji damu.
Wakati huo huo jumuiya ya Ujerumani inayotetea maslahi ya jamii zinazohatarishwa imemlaumu rais Horst Köhler kwa kumwalika waziri mkuu wa Ethiopia bwana Meles Zenawi kuhudhuria mkutano juu ya ushirikiano na bara la Africa .
Jumuiya hiyo imesema mji wa Bonn hauwezi kumkarimu kiongozi huyo wa Ethiopia,kutokana na kupigana vita ya kipuuzi dhidi ya Eritrea iliyosababisha vifo vya watu laki moja.Mkutano huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii hapa mjini Bonn ambapo viongozi watano kutoka Afrika wamealikwa.