ADDIS ABABA : Mkutano wa mgogoro wa Ivory Coast wafunguliwa
6 Oktoba 2005Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika PSC limeanza mkutano wa ngazi ya juu mjini Addis Ababa leo hii kusaidia kupanga jinsi Ivory Coast itakavyoongozwa baada ya tarehe 30 mwezi wa Oktoba tarehe ya uchaguzi wa Rais uliofutwa.
Mazungumzo hayo ya faragha ya siku mbili yamepangwa kulenga juu ya azimio la mkutano wa viongozi wa wiki iliopita wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ulioitishwa baada ya kubainika kwamba uchaguzi wa kumaliza mamlaka ya uongozi ya Rais Laurent Gbagbo hautoweza kufanyika na hiyo kuwacha pengo la kikatiba.
Mkutano huo wa leo unahudhuriwa na Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini,Olusegun Obasanjo wa Nigeria,Omar el Bashir wa Sudan na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi ambao wote ni wajumbe wa baraza hilo la amani na usalama barani Afrika PSC.
Gbagbo ambaye hapo Jumaatano alisema hatohudhuria mkutano huu na pia hakushiriki katika mazungumzo ya ECOWAS amemtuma mjumbe Addis Ababa ambapo Umoja wa Afrika AU una makao yake makuu.