Addis Ababa. Majeshi ya Ethiopia yashambulia Wasomali.
24 Desemba 2006Matangazo
Ethiopia imesema kuwa majeshi yake yameshambulia ndani ya ardhi ya Somalia dhidi ya majeshi ya mahakama za Kiislamu. Hii inafuatia madai ya umoja wa mahakama hizo kuwa ndege za kivita za Ethiopia zimeshambulia maeneo kadha, ikiwa ni pamoja na mji unaoshikiliwa na wapiganaji wa Kiislamu wa Beletweyne.
Mapigano , ambayo yameongezeka nchini Somalia tangu Jumatano iliyopita , yameripotiwa pia kutokea karibu na mji wa Baidoa, makao makuu ya serikali dhaifu ya mpito inayoungwa mkono na Ethiopia.
Ethiopia hapo kabla imesema kuwa imetuma wataalamu wa kulifunza jeshi la serikali. Majeshi ya wapiganaji wa Kiislamu yanadhibiti mji mkuu Mogadishu pamoja na maeneo kadha nchini humo.