ADDIS ABABA Machafuko bado yanaendelea nchini Ethiopia
8 Juni 2005Machafuko kati ya polisi wa kuzima ghasia na waandamanaji bado yanaendelea mjini Addis, Ethiopia. Mapema leo waethiopia wasiopungua wanane waliuwawa kwa kupigwa risasi na wengine 100 wakajeruhiwa wakati polisi wa kuzima ghasia walipokabiliana na waandamanaji wanaoyapinga matokeo ya uchaguzi wa mwezi uliopita nchini humo.
Wakati huo huo, mkurugenzi wa vipindi vya redio Deutsche Welle, Joachim Lens, ameikosoa hatua ya wizara ya habari nchini Ethiopia kufutilia mbali vibali vya waandishi habari wa redio Deutsche Welle, na shirika la VOA, akisema ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari.
Bi Assegedech Yiberta na bwana Tadesse Engidaw, ambao huripotia idara ya lugha ya Amharic ya redio Deutsche Welle, kuhusu matukio ya kisiasa nchini Ethiopia, na wenzao watatu wa shirika la VOA, wanatuhumiwa kwa kuripoti habari za uongo baada ya uchaguzi kufanyika. Lens amesema kwa serikali ya Ethiopia kuwatendea jambo kama hilo raia wake wenyewe ni kinyume cha demokrasia.
Wakati wa kampeni za uchaguzi huo wa Ethiopia, mwandishi habari mwingine wa redio Deutsche Welle, Tekla Yewhala, alikatazwa kufanya kazi yake nchini humo.