ADDIS ABABA : Kamata kamata yaendelea Ethiopia
11 Juni 2005Mji mkuu wa Ethiopia unaendelea kuwa katika hali ya wasi wasi huku maduka yakiwa yamefungwa na hakuna huduma za taxi kufuatia kuvunjwa na polisi kwa kutumia nguvu maandamano hapo Jumatano yaliopelekea kuuwawa kwa watu 26.
Chama kikuu cha upinzani cha CDU hapo jana kimesema wafanyakazi wake 37 zaidi wametiwa mbaroni na makamo wake mwenyekiti amepigwa marufuku kusafiri kwenda Uingereza.
Mashahidi mjini Addis Ababa wanasema polisi pia imekamata watu zaidi wakiwemo wanafunzi.Waziri Mkuu Meles Zenawi amesema kipindi kibaya kimepita na kuongeza kwamba anasikitika juu ya maisha yaliyopotea.
Chama cha CDU kimesaini na serikali makubaliano ya kuacha kutumia nguvu lakini kimeendelea kuwashutumu wanajeshi wa Zenawi kwa kunyanyasa watu.
Ghasia zilizuka nchini Ethiopia hapo Jumatatu kutokana na uchaguzi wa hivi karibuni uliozusha utata.
Balozi za kigeni 22 katika baruwa zimewataka wanajeshi wa Ethiopia kuonyesha uvumilivu wa kujizuwiya kuchukuwa hatua kadri inavyowezekana kwa wale waliowaita waandamanaji wa amani.