1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Afrika yashikilia msimamo wao juu ya mageuzi ya Umoja wa Mataifa

1 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CEN1

Viongozi wa Kiafrika hapo jana wameamuwa kuendelea kushinikiza kupatiwa kwa bara hilo viti viiwili vya kudumu vyenye uwezo wa kura ya turufu kama sehemu ya kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wakuu wa nchi na maafisa wa serikali kutoka nchi 48 za Afrika walikutana katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa kujadili na kuamuwa juu ya repoti ya viongozi 10 wa Afrika kuhusu msimamo inaopaswa kuchukuwa Umoja wa Afrika katika mageuzi ya Umoja wa Mataifa.

Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano huo wa siku moja imesema juu ya kwamba Afrika kimsingi inapinga suala la kura ya turufu maoni yake ni kwamba kwa kadri itakapoendelea kuwepo na kama ni suala la haki ya pamoja basi haki hiyo itolewe kwa wanachama wote wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Viongozi hao wa Kiafrika pia wamekubaliana kuunda kamati ya maafisa wa nchi 18 wanachama wa Umoja wa Afrika kuwasilisha azimio juu ya msimamo huo kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa wakati muafaka.

Afrika ni bara pekee lisilokuwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.