1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adai uchaguzi Afghanistan ulifanyiwa hila

24 Agosti 2009

Mpinzani mkuu wa rais Hamid Karzai nchini Afghanistan, amesema ana ushahidi wa kutosha kwamba kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/JHN0
Dr Abdullah AbdullahPicha: DW

 Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Abdullah Abdullah ameongeza kuwa amewasilisha malalamishi zaidi ya 100, akidai Rais Karzai aliiba kura katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alhamisi.

Siku ya alhamisi Wafghani walifanya maamuzi kupitia kura zao- katika uchaguzi wa pili wa rais nchini humo. Sasa lililosalia limo mikononi mwa tume ya uchaguzi- kuhesabiwa kwa kura. Ni zoezi linaloangaliwa kwa makini- huku tume ya uchaguzi nchini Afghanistan ikisema itaanza kutoa matokeo ya awali kuanzia hapo kesho.

Jinsi wagombea wote watakavyopokea matokeo rasmi ya uchaguzi- ni swala linalosubiriwa kwa hamu nchini Afghanistan na pia nchini Marekani- kutokana na kwamba Rais Obama ameweka swala la kuidhibiti Afghanistan kama mojawapo ya sera zake muhimu.

Rais Hamid Karzai na mpinzani wake mkuu- waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje- wote wamedai ushindi- hata kabla ya zoezi la kura kuanza- lakini taarifa kutoka Afghanistan zinasema wawili hao wataheshimu matokeo rasmi yatakapotangazwa.

Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi- kura mbili za maoni nchini humo zilionyesha rais Karzai huenda akashinda, lakini ushindi wake utakuwa na doa kwani hatopata idadi ya kura zinazotakikana kumzuia kuingia tena debeni katika duru ya pili dhidi ya mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah.

Mbali na kuwa amemtoa jasho rais Karzai- waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi za nje sasa anaelekeza kidole cha lawama kwa Karzai akisema uchaguzi wa alhamisi ulikuwa na udanganyifu mkubwa. Miongoni mwa malalamishi ya Abdullah ni kwamba baadhi ya maeneo kama Kandahar na Ghazni, yalirekodi idadi za uwongo za wapigaji kura, huku maafisa wa serikali wakiwalazimisha raia wa Afghanistan kumpigia kura kwa lazima rais Karzai- madai kambi ya Karzai imekana.

Tume ya malalamishi imethibitisha kupokea zaidi ya visa 200 vya malalamishi, lakini tume hiyo imesisitiza hili halitaathiri matokeo rasmi ya uchaguzi.

Huku Afghanistan ikisubiri matokeo ya uchaguzi wake, mkuu wa majeshi nchini Marekani Admiral Mike Mullen ametahadharisha kwamba hali ya usalama nchini Afghanistan  inazidi kuzorota, hasa kutokana na kwamba wapiganaji wa Kitaliban wameimarika kimashambulizi. Marekani imeongeza idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan, mkakati wa rais Obama kuwaangamiza wataliban- lakini uungwaji mkono wa vita hivyo miongoni mwa Wamarekani umeanza kupungua kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya wanajeshi wa Marekani nchini humo.

Mwandishi: Munira Muhammad/ rtre.

Mhariri:Aboubakary Liongo