AC Milan yamtimua kocha Allegri
13 Januari 2014Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya vigogo hao wa soka kuabishwa kwa kupewa kichapo cha mabao manne kwa matatu na klabu iliyopandishwa ngazi msimu huu Sassulo.
Huku wakiwa katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa ligi kuu ya Italia Serie A, Milan wametangaza uamuzi huo kupitia tovuti yao. Wameshinda mechi 19 pekee msimu huu na Allegry alikuwa tayari ametangaza katika kipindi kifupi cha mapumziko ya majira ya baridi kuwa huenda akaondoka mwishoni mwa msimu.
Allegri alichukua usukani mnamo mwaka wa 2010 na akashinda Serie A katika msimu wake wa kwanza kisha akamaliza katika nafasi za pili na tatu katika misimu iliyofuata. Hata hivyo, AC Milan ndio timu pekee ya Italia kufuzu kazika awamu ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na watapambana na Atletico Madrid mwezi ujao.
Kwingineko, barani Ulaya, Real Madrid waliitumia faida ya mchuano uliotoka sare kati ya viongozi wa La liga Atletico Madrid na Barcelona kwa kusajili ushindi wa goli moja kwa sifuri nyumbani kwa Espanyol na kupunguza pengo baina ya viongozi hao hadi pointi tatu pekee..wakati ikiwa imefikia nusu ya msimu. Bao la kichwa alililofunga Pepe lilitosha kuwapa Madrid pointi tatu na sasa wako katika nafasi ya tatu na pointi 47.
Kule England, Manchester City walisonga hali kileleni mwa Premier League, baada ya kupata ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Newcastle baada ya Chelsea kushikilia usukani kwa siku moja kufuatia ushindi wao wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Hull.
Arsenal waliteremka hadi nafasi ya tatu lakini leo wanaweza tena kurejea kileleni, kama watawashinda Aston Villa. Kwingineko magoli yalizidi kutiririka kwa upande wa Liverpool ambao wako katika nafasi ya nne, baada ya Luis Suarez kufunga mawili katika ushindi wao wa magoli matano kwa matatu dhidi ya Stoke.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman