Abidjan: Viongozi wa Afrika na Ulaya wakutana kuhusu ajira
29 Novemba 2017Zaidi ya viongozi 80 wa Afrika na Ulaya wanakusanyika mjini Abidjan-Cote d´Ivoire leo, kushajiisha juu ya ajira na utulivu kwa idadi inayozidi kuongezeka barani Afrika, huku baadhi wakitoa wito wa kuwepo mpango mpya wa uokozi sawa na ule uliobuniwa kuisaidia Ujerumani baada ya vita unaojulikana kama " Mpango wa Marshall."
Mkutano huo wa siku mbili mjini Abidjan unafunguliwa wakati Umoja wa Ulaya ukizidi kuona hatima yake ikifungamana na Afrika, kufuatia matukio mawili yasiotarajiwa-uhamiaji na mashambulizi ya kigaidi. Unafanyika wakati China, India, Japan na mataifa ya ghuba na mengineyo pia yakiwania ushawishi barani humo, ambako mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya kwa jumla yakisalia kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi na kisiasa .
Mamilioni ya nafasi za ajira zahitajika Afrika
Rais wa bunge la Ulaya mwanasiasa wa Italia Antonio Tajani aliwaambia wabunge kutoka abara yote mawili kabla ya mkutano huo wa kilele kwamba kuna muda mdogo mno wa kutafuta njia ya kuweza kukidhi mahitaji ya umma wa Afrika, ambao idadi yao itaongezeka maradufu ifikapo 2050 na kufikia watu bilioni 2.4. Tajani alisema Afrika inapaswa kuunda mamilioni ya nafasi za ajira kukabiliana na idadi mpya ya watu wake katika soko la ajira na kwamba ikiwa hilo halitatokea vijana watapoteza matumaini.
Akizungumza na DW kabla ya mkutano kwenye mji huo wa kiuchumi wa Cote d´Ivoire kuhusu hali ya vijana barani Afrika kuwa sawa na Bomu na ikiwa anafikiria viongozi wenzake kweli wanalielewa hilo, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Alpha Conde wa Guinea alisema:-
" Nimeyasema haya miaka minne sasa. Kuna haja ya kuwekeza kwa vijana kwa hiyo viongozi wote wa Afrika wanazingatia kwamba vijana vijana ndiyo matumaini yetu na pindi hakutakuweko na ajira kwa vijana , Afrika italipuka. Kwa hiyo viongozi wanaelewe juu ya haja ya kupambana na rushwa, kuekreza kwa vijana na utawala bora."
Mabilioni ya Euro kukuza maendeleo ya kiuchumi Afrika yatengwa
Umoja wa Ulaya umetenga mfuko wa mabilioni ya Euro kukuza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, wakati ukitanua zaidi ushirikiano na nchi za kiafrika katika kupambana na ugaidi katika bara hilo ambako makundi ya kiislamu ya siasa kali yanajitanua.
Balozi wa Morocco katika Umoja wa ulaya Ahmed Reda Chami pia ametoa wito wa kuwepoo mpango wa Marshall kwa ajili ya Afrika, lakini utakaolindwa na hatua dhidi ya rushwa na kuzingatia mahitaji ya Afrika. Itakumbukwa mpango wa Marshall wa mabilioni ya dola ulianzishwa na Marekani baada ya vita vya pili ya dunia, kulisaidia bara Ulaya kujikwamua kiuchumi na kuweza kufikia mafanikio makubwa na utulivu unaoshuhudiwa hii leo.
Mkutano huo wa kilele wa mataifa 55 ya Umoja wa Afrika na 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya huenda pia ukazungumzia matukio ya kushtusha ya wahamiaji kupigwa mnada huku wakiuzwa kama watumwa nchini Libya . Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afriaka Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa kuchuliwa hatua za dharura kuzuwia mtindo huo, ambao wakosoaji wanasema umetokana na kushindwa kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha kuzuwia wimbi la wahamiaji wenye kiu cha kuingia barani Uaya kwa kupitia Libya.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp
Mhariri:Josephat Charo