Abe awaomba radhi Wamarekani
30 Aprili 2015Wabunge wote wa Marekani walisimama jana Jumatano (Aprili 29) kumpokea kwa makofi mgeni wao huyo kutoka Japan, taifa ambalo mwezi Agosti mwaka 1945 jeshi la Marekani liliiangushia mabomu mawili ya atomiki katika miji ya Nagasaki na Hiroshima katika hatua za mwisho mwisho za kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.
Waziri Mkuu Abe aliitumia hotuba yake hiyo ya jana kuelezea kile alichokiita majuto makubwa kwa dhima ya Japan katika Vita hivyo vya Pili, ingawa wakati huo huo alisema nchi yake inainukia kuwa nguvu kubwa ya kiusalama barani Asia.
"Historia ni katili. Kilichofanywa hakiwezi kubadilishwa. Kwa majuto makubwa moyoni mwangu, nilisimama kwenye Mnara wa Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Pili wa Marekani nikiwa nasali kimoyomoyo. Marafiki zangu wapendwa, kwa niaba ya Japan na watu wa Japan, natoa mkono wa rambirambi kwa heshima na taadhima kwa roho za watu wote wa Marekani waliopotea wakati wa Vita vya Pili vya Dunia," alisema Abe huku akishangiriwa na wajumbe wa Congress.
Kwa upande mwengine Abe alisema Japana haipaswi kupuuzia mateso ya watu wa Asia kutokana na kile kilichofanywa na nchi wakati wa vita, lakini hakusema ikiwa nao pia anawaomba radhi, akisisitiza tu kuwa anasalia na msimamo uliowahi kutolewa na watangulizi wake.
Hasira za Wakorea
Kutokulitaja mahsusi suala hilo kumezichukiza sana Korea ya Kaskazini na Kusini, ambazo katika hali ya kushangaza sana, zimetoa kauli ya pamoja na kumlaani Waziri Mkuu huyo wa Japan. Mawaziri wa mambo ya nje wa Korea hizo mbili wametoa matamko ya kumkosoa Abe kwa kuipotosha historia, huku wa Korea Kaskazini ikifika umbali wa kumfananisha Abe na mwendawazimu.
Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini imesema ni bahati mbaya kwamba Abe ameshindwa kuitumia fursa hiyo adhimu kabisa kwenye bunge la Marekani kurekebisha historia na kujenga moyo mpya wa maridhiano kwa kile ambacho nchi yake ilikitenda kwa mataifa ya Asia wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Tahariri za vyombo kadhaa kwenye Korea zote mbili pamoja na China hivi leo zimemkosoa Abe kama kiongozi anayeendekeza sana utaifa wa nchi yake kwa gharama za kulitenga taifa hilo la Asia na majirani zake.
Akigusia kile alichokiita mzozo wa bahari za Asia, Abe alisema kwenye hotuba hiyo mbele ya Congress kwamba Japan inaamini kwenye kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa, majadiliano na njia za amani na sio matumizi ya vitisho na nguvu, akiikusudia bila kuitaja jina, China, ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na mzozo unaokaribia wa kijeshi na majirani zake kwenye Bahari ya Kusini.
Mbali na kubeba ajenda hiyo ya kihistoria, ziara ya Abe nchini Marekani inatazamiwa zaidi kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya washirika hao wawili kupitia mkataba wa biashara ya Pasifiki (TPP).
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba