Abbas na Netanyahu kutetea misimamo yao Umoja wa Mataifa
27 Septemba 2012Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Utawala wa Palestina, Mahmoud Abbas, atalihutubia Baraza Kuu ikiwa ni mwaka mmoja tokea alipotoa wito wake wa kihistoria mbele ya Baraza hilo juu ya kuwepo dola ya Palestina.
Safari hii anarudi tena akitaka Wapalestina wapewe hadhi ya kuwa dola mwangalizi asiye mwanachama kamili katika Umoja huo. Jaribio lake la mwaka jana kudai uwanachama kamili liligonga mwamba, baada ya kushindwa kupitishwa na Baraza la Usalama kwa sababu ya kikwazo cha Marekani.
Hata hivyo, mara hii hili la kutaka kutambuliwa kama mwanachama mtazamaji katika Umoja huo, lina nafasi kubwa kwa sababu ya wingi wa kura unaohitajika. Wakati panatakiwa idadi ya nchi 120 kati ya 193 kulipisha ombi hilo, tayari maafisa wa Palestina wanasema wanatarajia kati ya nchi 150 na 170 kuwaunga mkono. Lakini, bila ya shaka, si Marekani na Israel.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anapinga hata lengo hilo la Wapalestina, wakati ambapo mazungumzo ya ana kwa ana yamekwama tangu 2010, pale Wapalestina waliposema kwanza lazima ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi usimamishwe kabisa.
Netanyahu anakerwa zaidi na Iran kwa sasa
Hata hivyo, Netanyahu amewasili New York akiwa na mada nzito zaidi kwake, nayo ni wasiwasi unaozidi kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran, ambao Israel na nchi za Magharibi zinaamini una lengo la hatimaye kutengeneza silaha za kinyuklia.
Israel inasema mradi huo ni kitisho kwa Israel hasa kwa kuwa Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran ametamka bayana kuwa lengo la nchi yake ni kuiangamiza Israel. Netanyahu anasema Iran ni "nchi hatari kabisa duniani" na kwamba hilo atalitilia mkazo katika hotuba yake.
Israel inategemea sana uungaji mkono wa Marekani katika kuizuwia Iran kuwa na silaha ya nyuklia. Akilihutubia Baraza Kuu hapo Jumatatu, Rais Barack Obama alisema utawala wake utafanya kila uwezalo kuhakikisha Iran haifikii umbali huo.
Mbali na Iran, kwenye hotuba hiyo Obama pia alizungumzia Mashariki ya Kati akisisitiza tena msimamo wa nchi yake kuona linapatikana suluhisho la mzozo wa Israel na Palestina kwa kuwepo dola ya Wapalestina itakayoishi kwa amani na jirani yake Israel.
Rais Abbas ndiye anayetarajiwa kuwa wa kwanza kuzungumza na baadaye atafuata Waziri Mkuu Netanyahu.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AFP
Mhariri: Saumu Mwasimba