90 wasemekana wauwawa Afghanistan.
4 Septemba 2009Nchini Afghanistan, hujuma ya ndege za kivita za NATO imeteketeza meli mbili zilizopakia mafuta yaliotekwanyara na watalibani na wingu la moto uliozuka limeuwa kiasi cha watu 90 wengi wao ni wapiganaji wa kitalibani.
Kikosi cha kimataifa cha ISAF kinachoongozwa na shirika hilo la ulinzi (NATO), kimearifu kuwa kinachunguza taarifa za kuuwawa kwa raia katika hujuma hiyo. Taarifa ya jeshi la Ujerumani huko Kunduz, imetaja idadi ya waliouwawa ni 56 na kwamba hakuna raia miongoni mwao.
90 WAUWAWA ?
"Kiasi cha watu 90 wameuwawa katika hujuma hii na wengi wao ni wapiganaji wa Taliban. Ilikua hujuma iliofanywa na kikosi cha ISAF."-alisema Mahbubullah Sayedi, msemaji wa serikali ya jimbo la Kunduz.
Akaongeza kusema kwamba, idadi ndogo ya waliouwawa ni raia wa Kunduz miongoni mwao watoto wachache waliokwenda kwenye meli hizo kuchukua mafuta ya bure.Mkuu wa Polisi wa Kunduz ,Basharyal Parwani, amesema zaidi ya watu 60 wameuwawa na kujeruhiwa, Maafa ya raia katika hujuma za vikosi vya nchi za magharibi nchini Afghanistan ni swali nyeti na ndio chanzo cha mfarakano na serikali ya rais Hamid Karzai,anaeongoza katika matokeo ya uchaguzi wa rais unaotuhumiwa ulijaa mizengwe.
KIJIJI CHA YAQUBI:
Katika kijiji cha Yaqubi, mamia ya watu walikusanyika ili kuzika maiti 18 baadhi zikiiungua usoni hadi ilikua shida kutambulikana.
"Watu walikwenda kuchukua mafuta.Watalibani wakigawa mafuta ya bure. Ni hapo ndipo walipohujumiwa kwa mabomu. Watu 18 waliuwawa kutoka kijiji chetu." Alisema Azizullah mwenye umri wa miaka 45. Kiasi cha wanavijiji 200-250 inakisiwa walikusanyika kujipatia mafuta ya bure kutoka meli hizo-alisema msemaji wa wizara ya afya Farid Rahul,mjini Kabul.
Shahidi Mohammed Daud, mwenye umri wa miaka 32, alisema wanavijiji walilikimbilia gari moja la lori pale lilipokwama mtooni ili kujipatia mafuta ya bure wakiitikia mualiko wa Watalibani.
Msemaji wa ISAF alisema:
"Baada ya kuikagua hali ya mambo na kujua waasi wako eneo hilo,Kamanda wa ISAF wa eneo hilo aliamrisha hujuma hiyo ya ndege."
JESHI LA UJERUMANI:
Jeshi la Ujerumani ambalo wanajeshi wake wamepiga kambi huko Kunduz,chini ya uongozi wa shirika la NATO, limesema hujuma hiyo imeuwa watalibani 56 baada ya kuhujumu mlolongo wa shehena wa vikosi vya kimataifa. Likaarifu zaidi kwamba hakukuwa na raia waliouwawa wala dhara zozote kwa vikosi vya Ujerumani.
Mkasa huu umezuka siku 4 baada ya Kamanda wa Marekani na NATO nchini Afghanistan, kukabidhi mapendekezo ya kukaguliwa mkakati wa vita uliotumiwa miaka kiasi cha miaka 8 iliopita nchini Afghanistan. Aliitisha mageuzi katika juhudi za kuwashinda Watalibani na kuibadili hali mbaya ya Afghanistan. Mtangulizi wake Jamadari huyu Stanley McChrystal-jamadari David McKiernan, aliondoshwa katika wadhifa wake baada ya kutumika si zaidi ya mwaka .Hii ilifuatia hujuma ya kutatanisha iliouwa raia darzeni kadhaa magharibi mwa Afghanistan.