80 wauawa katika shambulizi Kabul
31 Mei 2017Hata hivyo, Msemaji wa wizara ya afya ya jamii wa Afghanistan, Wahidullah Majron amesema watu 80 waliuawa na 350 walijeruhiwa. Na hata lori lililotumika kwa shambulizi hilo nalo liliharibika vibaya, amesema Najib Danish, ambaye ni naibu msemaji wa wizara ya mambo ya ndani.
Kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya ndani, Magari 50 pia yaliharibiwa kwenye mripuko huo uliotokea katika eneo la Zanbaq Square, katika mji mkuu wa Afghanistan, ambako ni karibu na eneo lenye majengo mengi ya serikali na balozi za nchi mbalimbali, makazi ya rais ofisi ya waziri kiongozi, ubalozi wa Ujerumani, India na mengine mengi. Ubalozi wa Ujerumani umeharibiwa vibaya. Huku balozi za China na Uturuki nazo zikiharibiwa.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amelaani shambulizi hilo akiliita kama "shambulizi la woga lililofanywa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuwalenga watu wasio na hatia". Waziri Kiongozi Abdullah Abdullah alindika kupitia ukurasa wake wa Twitter "shambulizi la kigaidi mjini Kabul" na kusema anasimama pamoja na familia za wahanga wa shambulizi hilo.
Ubalozi wa Ujerumani ni moja ya balozi zilizoharibiwa vibaya. Mmoja wa walinzi wake aliuawa na baadhi ya watumishi kwenye ubalozi huo wamejeruhiwa vibaya. Waziri wa masuala ya kigeni wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema licha ya kuwaombea majeruhi wapone haraka, lakini mashambuliza kama hayo hayawezi kubadilisha dhamira ya Ujerumani kwa Afghanistan ya kuisaidia serikali ya nchi hiyo katika kuleta utulivu na maendeleo.
Pakistan nayo imelaani shambulizi hilo ililooita ni la kigaidi katika taarifa yake iliyotolewa na wizara ya mambo ya kigeni na kueleza kwamba itasimama pamoja na jirani yake huyo Afghanistan katika kipindi hiki.
Aidha, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amelaani vikali shambulizi hilo aliloiita kuwa ni la kutisha na kutuma salamu zake za pole kwa wahanga katika ujumbe wake alioutuma kupitia ukurasa wake wa twitter. Amesema shambulizi hilo linaashiria kupuuzwa kabisa kwa raia na maadui wenye ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Afghanistan.
Stoltenberg amesema shambulizi hilo pia linaashiria undumilakuwili wa maadui wa nchi hiyo wanaodai kwamba walidhamiria kuvilenga vikosi vya Afghanistan na vile vya nje, na badala yake kuendelea kusababisha mauaji na mateso kwa watu wasio na hatia.
Kundi la wapiganaji wa Taliban liliko Afghanistan limepinga kuhusika na shambulizi hilo. Msemaji wake Zabihullah Mujahid amesema kwenye taarifa yake kwamba wapiganaji wake hawahusiki kwa namna yoyote, na wao pia wanalaani vikali mashambulizi yoyote yanayosababisha adha kwa raia.
Ubalozi wa India hakuathirika na watumishi wake wako salama, amesema waziri wa masuala ya kigeni wa India Sushma Swaraj kupitia ukurasa wake wa Twitter. Ubalozi wa Marekani ulioko Kabul, karibu na eneo hilo lililoshambuliwa umewataka raia wake kutofika katika eneo hilo na kufuta miadi yote iliyopangwa kufanyika leo.
Mwandishi: Lilian Mtono/dpae/Rtre/Ape.
Mhariri: Yusuf Saumu