1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

250 wahofiwa kuzama Mediterrania

Iddi Ssessanga24 Machi 2017

Zaidi ya wahamiaji 250 wanahofiwa kuzama katika Bahari ya Mediterrania jana Alhamisi baada ya boti ya msaada ya uokozi kugundua miili mitano iliyokuwa karibu na boti mbili zilizokuwa zinazama katika pwani ya Libya

https://p.dw.com/p/2ZsGr
Libyen Tote Flüchtlinge an der Küste nahe Zawiya
Picha: picture-alliance/AP Photo/IFRC/M. Karima

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema hali hiyo iliibua wasiwasi, baada ya boti ya uokozi ya Golfo Azzuro inayoendeshwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Hispania, ya Proactiva Open Arms kuarifu kugundua miili hiyo iliyokuwa karibu na boti iliyokuwa imevutwa na mkondo wa maji ikikaribia kuzama, maili 15 kutoka pwani ya Libya.

Msemaji wa taasisi hiyo ya Proactiva Laura Lanuza ameliambia shirika la habari la AFP wanadhani kwamba boti hizo zilizopasuka zilikuwa zimefurika watu, na wana hofu kwamba wanaweza kuwa wamezama. Amesema boti kama hizo hutumiwa na watu wanaofanya biashara haramu ya usafirishaji binadamu, na hubeba kati ya watu 120-140.

Lanuza amesema, miili iliyopatikana ni ya wanaume wa kiafrika, wanaodhaniwa kuwa na kati ya miaka 16 na 25, walizoama katika kipindi cha masaa 24 kabla ya kugundulika kwa miili hiyo jana.

Mkurugenzi wa UNHCR ofisi ya Ulaya, Vincent Cochetel amesema, boti hiyo ya Proactiva iliyokuwa ikifanya doria katika eneo hilo iliomba msaada kwa ajili ya boti ya tatu iliyopigwa na mawimbi ya maji jana mchana, na kuzua hofu ya uwezekano wa watu wengine kusombwa na maji. Hofu hiyo imelifanya shirika hilo kuiita siku hiyo kuwa "Siku ya kiza ndani ya Mediterrania".

Mittelmeer Flüchtlingsboot
Wahamiaji wakiwa kwenye boti ya mpira wakisubiri kuokolewa katika bahari ya MeditterraniaPicha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Mnamo siku ya Jumatano Mkurugenzi mkuu wa shirika la uhamiaji duniani, IOM William Swing aliwasili mjini Tripoli, Libya na kukutana na maafisa wa nchi hiyo kujadili kuhusu suala la uhamiaji ndani ya nchi pamoja na watu waliokimbia makazi. Alisema ziara yake ilillenga kuendeleza uungaji mkono wa shirika hilo nchini Libya kwa kuangazia zaidi makambi ya kuwazuia wahamiaji na kuwapa msaada mamia kwa maelfu ya raia waliokimbia makazi yao.

Naibu Waziri wa masuala ya kigeni wa Libya Lufti Al-Magrabi alielezea matarajio yake juu ya ushirikiano kati yao na IOM katika kumaliza tatizo la wahamiaji ambalo limesababisha matatizo nchini humo na Barani Ulaya.

Karibu watu 6,000 wameokolewa na boti za uokozi zinazoratibiwa na Italia tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, na kufanya idadi ya wahamiaji waliookolewa nma boti hizo tangu mwanzoni mwa mwaka huu kufikia 22,000, na idadi hii ikiwa imepanda tofauti na kipindi kama hiki miaka iliyopita.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP.

Mhariri:Iddi Ssessanga