20,000 wakimbilia Ethiopia kwa sababu ya mapigano Sudan
7 Septemba 2011Vurugu hizo zinatokea ikiwa ni siku moja baada ya gavana mpya wa kijeshi kutangaza kuwa hali ni shwari. Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita, maelfu ya watu walilazimika kuyakimbia makaazi yao baada ya mapigano kuzuka kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa kundi la Sudan People's Liberation Movement, SPLM.
Umeme wakatika
Milio ya risasi ilisikika jana jioni kwenye eneo la Blue Nile la Sudan lililoko mpakani. Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Reuters aliyekuwa kwenye mji mkuu wa Damazin, huduma za umeme zilisitishwa kwa muda baada ya mapigano hayo kutokea katika baadhi ya maeneo ya mji.
Duru za kijeshi zinaeleza kuwa mwanajeshi mmoja kwenye eneo hilo alifyatua risasi kwa bahati mbaya, kitendo kilichowachagiza wanajeshi wengine kuufuata mkondo huo. Taarifa hizo zimethibitishwa na shirika rasmi la habari la Sudan la SUNA.
Mpaka wawaka moto
Kulingana na msemaji wa jeshi la Sudan aliyezungumza na shirika hilo, hali kwa sasa ni shwari na hakuna majeruhi wowote. Hata hivyo hakuna kauli yoyote iliyotolewa na wapiganaji walio na mafungamano na kundi la SPLM-N. Kundi hilo lilijitenga na chama tawala cha eneo la Kusini mwa Sudan cha SPLM.
Maeneo ya Blue Nile na Kusini mwa Kordofan yaliyoko mpakani yamekuwa yakizongwa na mapigano makali katika kipindi cha miongo mingi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali kuu iliyo na makao yake mjini Khartoum na Kusini mwa Sudan.
Hatima ya maeneo ya Abyei kuliko na utajiri wa mafuta na Blue Nile yaliyoko mpakani bado haijaamuliwa mpaka sasa. Mjumbe maalum wa Marekani kuhusu Sudan, Balozi Princeton Lyman anausisitizia umuhimu wa kudumisha amani katika kipindi hiki na anasema ," Tumewaeleza washirika wa pande zote mbili kuwa wasihusike katika vitendo vya uchochezi kwani vinaweza kuivuruga hali kwa jumla na ikiwa yupo mshirika anayeyafanya hayo lazima wakome.Athari za vitendo hivyo zitawavuruga wahusika wa pande zote."
20,000 wakimbilia Ethiopia
Itakumbukwa kuwa mwaka huu, mapigano makali yameripotiwa kutokea katika maeneo yote matatu ambayo ni makaazi ya jamii za makabila yanayoliunga mkono eneo la Kusini mwa Sudan. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi, UNHCR, wakaazi hao wamekuwa wakikimbilia nchi ya Ethiopia tangu wiki iliyopita. Fatoumata Lejeune- Kaba ni msemaji wa UNHCR na anaielezea hali halisi: " Bado wanahitaji makaazi na maji safi. Kwa sasa kunanyesha na kuna baridi kwahiyo tunalazimika kufanya kila tuwezalo kwa haraka ili kuwasaidia kwa sasa."
Kwa upande wake, serikali kuu ya Sudan imekuwa ikiwalaumu wakaazi hao kwa kuhusika na vitendo vya uchochezi vinavyoungwa mkono na serikali ya Sudan Kusini kwenye eneo hilo la mpakani. Hata hivyo serikali ya Sudan Kusini inayakanusha madai hayo.
Wakati huohuo, makundi ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanailaumu serikali kuu ya Sudan kwa kujaribu kuwavuruga wapinzani waliosalia kadhalika kuchochea ghasia kwa kuwapokonya silaha wapiganaji wa makundi yaliyo na mafungamano na Sudan Kusini.
Gavana mteule
Wiki iliyopita, Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir alimteua Yahia Mohammed Kheir, kuwa gavana wa muda wa eneo la Blue Nile baada ya kumfukuza kazini gavana Malik Agar wa chama cha SPLM-N aliyechaguliwa.
Watu 12 wakiwemo wanajeshi, polisi 6 na raia watatu wa kawaida wameuawa tangu mapigano hayo yaanze wiki iliyopita mjini Damazin. Hapo jana, afisa wa ngazi za juu katika chama tawala cha serikali kuu ya Sudan cha NCP, Mandour al- Mahdi, alisema kuwa kundi la SPLM litalazimika kuzisitisha harakati zake za kisiasa katika eneo la kaskazini kwani halijsajiliwa rasmi.
Kwa upande wao, katika taarifa yake, katibu Mkuu wa kundi hilo, Yasir Arman, alisema kuwa uongozi unazifunga afisi zao kote nchini humo.
Itakumbukwa kuwa eneo la Kusini mwa Sudan lilijitenga rasmi na eneo la kaskazini na kuwa taifa huru mwezi Julai mwaka huu baada ya kura ya maoni kuiidhinisha hatua hiyo kama yanavyoeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005. Makubaliano hayo yalivimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-RTRE/AFPE/ Aljazeera & UN Multimedia
Mhariri:Josephat Charo