200 wauwawa vijijini Nigeria
17 Machi 2014Mauaji hayo yanayotokana na mizozo ya malisho, n'gombe na dini yanayoendelea kupamba moto nchini Nigeria.
Katika kadhia zote mbili wafugaji wa kabila la Fulani wanashukiwa kuhusika na mashambulio hayo.Msemaji wa polisi amethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo vijijini lakini hakutowa idadi ya maafa. Idadi ya watu 200 waliouwawa imezingatia makadirio ya idadi ya wahanga katika kila kijiji. Imeripotiwa kwamba washambuliaji kadhaa wakiwa na silaha nzito waliingia katika vijiji vya Ungwar Sankwai, Ungwar Gala na Chenshyi hapo Jumamosi.Mkaazi mmoja wa kijiji cha Chenshyi Nuhu Moses amekaririwa na kituo cha habari cha Nigeria CKN akisema nyumba zote zimeteketezwa na watu waliojaribu kukimbia waliuwawa kwa kupigwa risasi. Wahanga ni pamoja na mchungaji na wanawe.
Chifu mmoja wa jadi ambaye amekataa kutaja jina lake kwa kuhofia kushambuliwa amesema wanaume na wanawake, watoto na wazee waliuwawa kwa kupigwa risasi na kukatwa kwa mapanga wakati wengine waliteketezwa na moto majumbani mwao.
Chifu huyo amewaambia waandishi wa shirika la habari la Sahara kwamba pia watu wao wengi wamechukuliwa misituni na washambuliaji hao kutoka vijiji vyote.
Wahusika kusakwa
Gavana wa jimbo la Kaduna Mukhtar Ramalan Yero ameapa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wahusika wa mauaji hayo na ameamuru kufanyika kwa uchunguzi kamili na polisi tayari wametumwa kwenye vijiji vilivyoathirika na mashambilizi hayo.
Kaduna Kusini imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wafugaji wa kabila la Fulani tokea kuzuka kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2011.
Shambulio la Jumamosi limekuja katika kipindi kisichozidi saa 24 baada ya shambulio kama hilo katika jimbo la Benue ambapo washambuliaji wanaotuhumiwa kuwa wa kabila la Fulani walivamia vijiji kadhaa na kuuwa watu zaidi ya 30.
Mauaji yanaendelea
Mapema wiki hii washambuliaji wanaoaminika kuwa wezi wa n'gombe wa kabila la Fulani waliuwa takribani watu 133 katika vijiji kadhaa kwenye jimbo la Katsina.
Mamia ya watu wameuwawa mwaka jana katika mapambano kati ya wachunga n'gombe wa kabila la Fulani ambao wengi wao ni Waislamu na jamii za Wakristo kama vile za kabila la Berom katika eneo tete la Nigeria ya kati ambapo ndipo sehemu kubwa ya Wakristo wa kusini inapokutana na Waislamu wa kaskazinii.
Machafuko ya Nigeria ya kati kwa kawaida hayahusiani na uasi wa kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki ya Nigeria lakini wachambuzi wanahofia kundi hilo lenye mafungamano na kundi la Al Qaeda linalotaka kutumika kwa sheria kali za Kiislamu kaskazini mwa Nigeria linaweza kuutumia mzozo wa Nigeria ya kati kwa faida yao.
Mwandishi: Mohamed Dahmand/dpa/Reuters/
Mhariri: Mohammed Khelef