10 wauawa katika mapigano nchini Chad
27 Mei 2023Kulingana na taarifa ya gavana wa mkoa wa Madoul, Adoum Forteye, katika tukio la hivi karibuni lililotokea Alhamisi, mtoto wa kiume mwenye miaka 12 kutoka jamii ya wafugaji aliwapeleka wanyama na kuwalisha katika shamba la mkulima wa karanga hali iliyoibua ugomvi uliosababisha kifo cha kijana huyo.
Katika hatua ya kulipa kisasi, wazazi wa kijana huyo waliwauwa wakulima tisa tukio lililotokea katika kijiji cha Bara II kilomita 600 kusini mashariki mwa mji mkuu N'Djamena. Kufuatia tukio hilo, wafugaji watano pamoja na mtu anayetuhumiwa kumuuwa mtoto huyo wamekamatwa.
Mara nyingi wakulima wamekuwa wakiwatuhumu wafugaji kwa kulisha mifugo mazao yao na kuyaharibu huku wafugaji wakisema kwamba wana haki ya asili ya kuilisha mifugo kwenye maeneo hayo.
Machafuko ya aina hiyo yamekuwa yakiyatatiza maeneo yenye rutuba ya mpakani nchini Chad, Kameruni na Jamhuri ya Afrika ya kati.